MKUTANO WA KATIBU TAWALA WA MKOA WA PWANI NA WATUMISHI WA SERIKALI WILAYA YA KISARAWE.
Kisarawe, 18 Agosti 2025 – Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Pili Mnyema. leo ameongoza mkutano muhimu na watumishi wa umma katika Wilaya ya Kisarawe, akisisitiza masuala ya uadilifu, uwajibikaji, na maadili katika utumishi wa umma.
Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wakuu wa idara, pamoja na watumishi kutoka sekta tofauti. Katika hotuba yake, Katibu Tawala alitoa wito kwa watumishi wote kuzingatia viwango vya juu vya maadili ya kazi na kutekeleza wajibu wao kwa uaminifu na weledi mkubwa.
> “Uadilifu ni msingi wa utumishi wa umma. Serikali haiwezi kufanikisha mipango yake ya maendeleo bila watumishi wenye maadili, waaminifu na wawajibikaji,” alisema Bi.Pili mnyema.
Aidha, alikemea vitendo vya uzembe kazini, matumizi mabaya ya rasilimali za umma, pamoja na tabia za rushwa ambazo zinaathiri utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Aliwahimiza watumishi kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zote za kiutumishi.
Katika mazungumzo yake na washiriki wa mkutano, Katibu Tawala alisisitiza umuhimu wa kuwahudumia wananchi kwa heshima, upendo na ufanisi ili kukuza imani yao kwa serikali.
![]() |
![]() |
Mkutano huo ulihitimishwa kwa katibu tawala wa wilaya ya kisarawe Bi. Sara ngwele kumshukuru katibu tawala wa mkoa wa pwani kwa ujio wake wilayani kisarawe katika kutembelea miradi mbalimbali ya serikali wilaya ya kisarawe, aidha aliendelea kushukuru kwa Kusisitiza juu ya uwajibikaji na uadilifu wenye ufanisi kwa watumishi wa kisarawe.
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa