HALMASHAURI YA WILAYA YA KISARAWE YAFANYA KIKAO KAZI CHA WADAU WA MAENDELEO.
Leo Jumanne 15/12/2020, Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe imefanya kikao kazi kilichoshirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo, kwa ajili ya kujadili vipaumbele vya Mpango na Bajeti ya Halmashauri mwaka wa fedha 2021/2022 pamoja na michango ya wadau katika kuchangia vipaumbele vya Mpango na Bajeti hiyo, kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri uliopo Mtaa wa Bomani, Kata ya Kisarawe, Mkoani Pwani.
Kikao hicho kilifunguliwa na Mgeni rasmi Mhe. Jokate Mwegelo kwa kuwakaribisha wajumbe katika kikao kazi.Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Ndg. Mussa Gama, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho aliwataka wajumbe washiriki bila hofu katika kikao hicho ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa Kisarawe na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Jokate alianza kwa kuwakaribisha wadau wote waliohudhuria kikaoni, na kutoa nasaha zake zikiwemo kusisitiza usimamizi wa masuala ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Pia, alitilia mkazo suala la utendaji kazi wa mashirika binafsi, na taasisi zote zisizo za kiserikali kutoa taarifa mapema ili waweze kupata ushirikiano mzuri katika utendaji kazi wao.
Aidha, Ndg. Mwanana Msumi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kisarawe alizitaka asasi na taasisi zinazoshirikiana na Halmashauri kutoa ushirikiano, na mawasiliano ambayo ni nyenzo nzuri katika utekelezaji wa mambo mbalimbali yanayopelekea ustawi wa Halmashauri na Taifa kwa ujumla.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Ndg. Zuberi Kizwezwe alizishukuru taasisi na asasi zote kwa kutoa ushauri na mapendekezo, pia alitoa rai kwa taasisi na asasi hizo kuendelea kusaidia jamii, na kuvumilia changamoto zote kwa kushirikiana na Halmashauri.
Sambamba na hilo, Dokta. Casian, ambaye ni Afisa Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Kisarawe, alitoa angalizo kwa wadau waliohudhuria kikaoni hapo kutoa elimu kwa jamii kuhusu kuwalinda watoto dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa ambao hauna tiba, na chanjo yake ni aghali sana ambapo hupelekea madhara makubwa kutoa katika jamii ikiwemo watu kupoteza maisha.
Vilevile, Bi. Jesca Petro, mdau kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Plan International-Kisarawe aliahidi kuwa taasisi hiyo itaendelea kutoa huduma kwa jamii zikiwemo ujenzi wa vyoo, madarasa na visima, pamoja na mafunzo ya ulinzi na haki za watoto katika Kata mbalimbali zilizomo wilayani humo.
Imetolewa Na:
KITENGO CHA TEHAMA NA UHUSIANO
HALMASHAURI YA WILAYA YA KISARAWE
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa