KIKAO CHA WARSHA YA KUZUIA UKATILI DHIDI YA WATOTO WALIOKATISHA MASOMO WILAYA YA KISARAWE MWAKA 2025.
Kisarawe,
Leo 29/08/2025 kumefanyika Mkutano uliohusu masuala Katika juhudi za kuimarisha ulinzi wa watoto na kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto waliokatisha masomo, warsha maalum ya kuwajengea uwezo wasaidizi wa kisheria (paralegals) na wadau mbalimbali wa ulinzi wa mtoto imefanyika wilayani Kisarawe, mkoa wa Pwani.
Warsha hiyo iliratibiwa na shirika la Children Education Society (CHESO), likiongozwa na Advocate Richard Shilamba ambaye pia alikuwa mwenyeji wa kikao hicho muhimu. Warsha iliwakutanisha wasaidizi wa kisheria, maafisa ustawi wa jamii, walimu na mashirika ya kiraia yanayojihusisha na masuala ya watoto.
![]() |
![]() |
Mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa Bi. Esther Senkoro, Afisa Elimu wa Elimu ya Watu Wazima Wilaya ya Kisarawe, ambaye alisisitiza umuhimu wa kushirikiana kwa wadau wote katika kuhakikisha watoto waliokatisha masomo kwa sababu ya ukatili au changamoto nyingine wanapata fursa ya kurejea shuleni au kupata msaada unaofaa.
> "Ulinzi wa mtoto ni jukumu la jamii nzima. Tunapaswa kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma kwa sababu ya ukatili, mimba za utotoni au mazingira magumu ya kifamilia. Kupitia warsha hii, tunatarajia wasaidizi wa kisheria na wadau wa ulinzi wa mtoto kuwa na maarifa na mikakati madhubuti ya kusaidia watoto hawa," alisema Bi. Senkoro.
![]() |
![]() |
Advocate Richard Shilamba alieleza kuwa lengo kuu la warsha hiyo ni kuwajengea uwezo wasaidizi wa kisheria kuhusu sheria na mbinu bora za utetezi wa haki za watoto, hususan wale waliokatisha masomo kutokana na ukatili wa aina mbalimbali kama vile ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni, ajira hatarishi, na unyanyasaji wa majumbani.
Warsha hii ni sehemu ya mpango mpana wa CHESO wa kuimarisha ulinzi wa watoto katika jamii na kuhakikisha haki zao zinalindwa kupitia mifumo ya kisheria na kijamii.
Katika kikao hicho, washiriki walipata fursa ya kujadili changamoto zinazowakabili watoto waliokatisha masomo, kuandaa mikakati ya kusaidia watoto hao kurudi shuleni au kupata stadi za maisha, na pia kuunda mtandao wa kushirikiana katika kushughulikia kesi za ukatili dhidi ya watoto katika ngazi ya jamii.
Warsha hiyo imepokelewa kwa shukrani kubwa na washiriki, ambao walionyesha utayari wa kutumia maarifa waliyopata katika kusaidia watoto ndani ya jamii zao.
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa