Kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu ya Tanzania ya Viwanda Inawezekana Panda Miti Kwa Meandeleo Ya Viwanda Wilaya ya Kisarawe imejipanga kuchukua hatua mbalimbali za upandaji, utunzaji na ulindaji wa misitu kwa ajili ya faida ya ujumla kwa nchi.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Ndugu Mussa L Gama wakati wa maadhimisho a siku ya Upandaji miti iliyofanyika kwenye msitu wa Kazimzumbwi kata ya msimbu Wilaya ya Kisarawe.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng. Evarist Ndikilo mkurugenzi Mtendaji amesema sehemu kubwa ya rasilimali misitu imeharibiwa kutokana na uvamizi wa misitu kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu kama kilimo,uchomaji mkaa,na upasuaji mbao na ili kuirejesha misitu katika hali nzuri Halmashauri inatia juhudi kuhakikisha misitu iliyopo inasimamiwa vizuri.
Mikakati ilyowekwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ni kuipa shughuli ya upandaji miti kipaumbele na kuendelea kutoe elimu ya kutunza misitu ya asili na kuzingatia uvunaji endelevu wa mazao ya misitu.
‘’kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu Wilaya imeanzisha vitalu vikubwa vitatu katika kata ya Kisarawe,Mzenga na Kurui ambapo jumla ya miche 150,000 imezalishwa na imeshaanza kusambazwa na kupandwa maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wengine ambao ni Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),Asasi za dini na WWF ambao ni Mfuko wa dunia wa Kuhifadhi Viumbe Pori’’ Amesema Ndugu mussa Gama.
Aidha katika kukabiliana na changamoto mbalimbali hususani uvamizi,uvunaji holela na uchomaji wa mapori na misitu ya Hifadhi Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kisarawe imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana nazo ikiwamo kufanya doria maeneo mbalimbali,kuimarisha zoezi la upandaji miti kwa kushirikiana na kamati za mazingira za vijiji,kukamata wavamizi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria na kutoa elimu ya moto na athari zake kwa misitu kwa vijiji vinavyozunguka misitu ya Hifadhi.
Wilaya ya Kisarawe ina misitu ya aina tatu ambayo ni ile inayosimamiwa na Serikali kuu ambayo ni Pugu,Kazimzumbwi,Ruvu kusini na Masanganya.Pia ipo misitu inayosimamiwa na Serikali za vijiji ambayo ni Nyani,Kidugalo,Msanga Sokoni, Kisangire,Mafumbi,Sofu na Maharage Gwata.Aidha misitu ya asili shughuli za uvunaji wa mazao ya misitu hufanyika ni pamoja na Gwata -kidunda,Gwata –Mzenga,Kihare-Marui na vikumburu yenye jumla ya ukubwa wa Hekta 194,111. By dkambanyuma
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa