Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe imeadhimisha siku ya mtoto wa Afrika katika sherehe zilizofana zilizofanyika katika kata ya Masaki kijiji cha sungwi kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Sungwi.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Kisarawe yaliongozwa na Katibu tawala wa Wilaya ya Kisarawe ndugu Mtela Mwampamba ambaye alikuwa ni mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo.
Akihutubia hadhara iliyojumuika kwenye maadhimisho mgeni rasmi ametoa pongezi nyingi kwa taasisi ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kushughulikia masuala ya watoto kwa kuwajali,kuwalinda na kuwahudumia kwenye mahitaji yao muhimu na ya msingi.
‘’ Napenda kutoa pongezi kwa taasisi zote mnaojihusisha na kuwaendeleza watoto ili waweze kufikia malengo yao na malengo ya Serikali yaliyokusudiwa ya kumjenga mtoto,tunawashukuru shirika la Feed the Children,Plan Internation,Hope for young Girls,SHIVYAWATA kwa kuwajali na kuwasaidia watoto wetu’’ alisema Katibu Tawala Ndugu Mtela Mwampamba.
Aidha Katibu Tawala amewaambia wanafunzi na watoto waliohudhuria maadhimisho hayo wasome kwa bidii na hasa masomo ya sayansi ili kwenda sambamba na kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ya ‘KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA,TUSIMWACHE MTOTO NYUMA’ na ametoa taarifa kuwa Wilaya ya Kisarawe inaongoza kwa watoto wanaopata mimba kwenye Mkoa wa Pwani.
Wakisoma salamu zao kwenye maadhimisho,mwakilishi wa taasisi ya Plan Internation amesema mtoto anastahili kulindwa ,anastahili kuishi salama, na kusoma.Mwakilishi wa Feed the children amesema lishe ianze kutolewa tangu awali wakiwa watoto.’’siku elfu moja za mwanzo kwa watoto ni muhimu sana kwa kupewa lishe bora ,kwani asilimia arobaini na mbili ya watoto wamedumaa na ndiyo maana sisi tunahusika zaidi na kuhakikisha watoto wanapata elimu, lishe na kuboresha maisha yao’’ amesema mwakilishi huyo.
Aidha Mkurugenzi wa shirika la Hope for young Girls ametoa hamasa kwa watoto kusoma kwa bidii na wazingatie ujumbe na maudhui yaliyomo kwenye kauli mbiu ya mwaka huu inayohusu uchumi wa viwanda isimwache mtoto nyuma.Katika maadhimisho hayo shirika hilo limetoa msaada wa wa boksi za katoni kumi na tano za taulo za kike kwa ajili ya matumizi kwa wanafunzi wa kike.
Wakiwa kwenye maandamano ya kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika,watoto walioandamana walipaza sauti zao kwenye mabango waliyoyabeba yakisomeka kuwa ‘wazazi Mtulinde Tufikie Ndoto Zetu’ ‘Watoto Tunapinga Ndoa Za Utotoni’’Watoto Tuna Haki Ya Kusikilizwa’ pamoja na ‘Jamii Saidia Kutokomeza Mimba Za Utotoni’.
Maadhimisho hayo pia yamehudhuriwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Mheshimiwa Hamisi Dikupatile,Diwani wa Kata ya Masaki mhe.Pili Chamguhi na Diwani wa viti maalumu Tarafa ya Sungwi mhe. Valeriana Mkoka pamoja na wanafunzi wa shule mbalimbali na wananchi
By dkambanyuma
Copyright ©2017 Kisarawe District Council . All rights reserved.