MWANANCHI ATOA EKARI 20 BURE ZA UJENZI WA SHULE
Mdau mkubwa wa maendeleo katika sekta ya Elimu Wilayani Kisarawe ndugu Salum Zaga amekabidhi eneo lenye ukubwa wa ekari ishirini (20) kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari katika kata ya Kazimzumbwi Wilaya ya Kisarawe.
Ndugu Salum Zaga amekabidhi ekari hizo mbele ya Diwani wa Kata ya Kazimzumbwi Mheshimiwa Siza Juma aliyeongozana na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe akiwemo Afisa elimu sekondari ndugu Generosa Nyoni, Afisa elimu ndugu Alice Nkwera pamoja na Afisa Habari ndugu David Kambanyuma pamoja na Mratibu elimu na Afisa mtendaji wa Kata ya Kazimzumbwi.
Wakati wa makabidhiano hayo mdau huyo wa maendeleo ya elimu amewaambia Mheshimiwa Diwani na wataalamu wa Halmashauri wachague eneo linalofaa kwa ajili ya ujenzi wa shule kutoka miongoni mwa ekeri kadhaa anazozimiliki.
‘’Mheshimiwa Diwani Tafadhali chagueni eneo lolote mnaloliona linawafaa kwa ajili ya ujenzi wa shule na mimi nipo tayari kuwapa eneo hilo ‘’ Amesema ndugu Salum Zaga.
Eneo ambalo limekabidhiwa lipo karibu na barabara inayoelekea tarafa ya Mzenga na inakaribiana na barabara ya Reli ya TAZARA ambayo kwa kiasi ki kubwa inarahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii ikiwamo usafiri.
Kata ya Kazimzumbwi ni Kata ambayo haina shule ya sekondari ambapo wanafunzi wanalazimika kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kufuata elimu hiyo kwenye shule za sekondari Kimani na Chanzige zilizopo Kata ya Kisarawe.
Mdau wa maendeleo Ndugu Salum Zaga kwa muda mrefu amekuwa akichangia maendeleo ya elimu kwa muda mrefu ambapo hivi karibuni wakati wa zoezi la OPERESHENI ONDOA ZERO iliyokuwa na lengo la kuwaweka pamoja wanafunzi wa sekondari wanaojiandaa kufanya mitihani ya kumaliza elimu ya sekondari ameweza kuchangia kiasi cha shilingi miliono kumi (10) kwa ajili ya zoezi hilo.
Habari zaidi kwa njia ya picha Bonyeza hapa.pdf
Copyright ©2017 Kisarawe District Council . All rights reserved.