Kisarawe ni moja kati ya halmashauri tisa za mkoa wa Pwani.Imeanzishwa tarehe 1 Julai 1907.Wilaya ya Kisarawe inapakana na Wilaya ya Mkuranga kwa upande wa Kusini-mashariki na Wilaya ya Morogoro upande wa Magharibi.Mashariki-Kaskazini kuna Jiji la Dar es Salaam, Kaskazini Wilaya ya Kibaha na Kusini Wilaya ya Rufiji.
Wilaya ina eneo la ukubwa wa Kilomita za mraba 3535 na mita1000 juu ya usawa wa bahari.
Kiutawala Wilaya ya Kisarawe imegawanyika katika tarafa nne(4) ambazo ni Sungwi, Maneromango, Mzenga na Cholesamvula Wilaya ina jimbo moja la uchaguzi la Kisarawe.Jimbo hili kwa sasa linaongozwa na Mbunge wa kuchaguliwa Mhe. Dkt. Selemani Jafo ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na Mhe. Zaynab Vulu mbunge Viti Maalumu. Kwa upande wa uwakilishi wa Wananchi,Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ina jumla ya Madiwani 25.
Wananchi wa Kisarawe wanajishughulisha katika kilimo,Ufugaji na uchimbaji wa madini.
Hali ya hewa ni ya joto la wastani wa nyuzi joto 29°C. Mvua hunyesha kwa misimu miwili ya vuli (kuanzia Oktoba hadi Januari) na masika kati ya Machi na Juni kwa mwaka.Hali ya hewa ni nzuri kwa kilimo na Ufugaji wa mazao ya aina yote. Wastani wa mvua kwa mwaka ni mm 1,000.Pia kuna maeneo ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji.