Wananchi wa Mkoa wa pwani wameshauriwa kujisajili kwa Wakala wa huduma za misitu (TFS) ili wapate vibali kisheria na kuvuna rasilimali za misitu zinazopatikana katika mkoa wao.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng.. Evarist Ndikilo wakati wa maadhimisho ya siku ya upandaji miti kimkoa zoezi ambalo limefanyika katika msitu wa hifadhi wa Kazimzumbwi unaopatikana katika Wilaya ya Kisarawe.
Eng. Ndikilo amesema kuwa wananchi wengi wa Mkoa wa Pwani ndio wanalinda na kutunza misitu lakini wengi wanaonufaika rasilimali zitokanazo na misitu hiyo ni watu kutoka nje ya mkoa wa pwani.Amebainisha kuwa kuna watu na makampuni 389 wamejisajili kwa ajili ya kuvuna na kutumia rasilimali hizo lakini wengi wanatoka nje ya Mkoa wetu wa Pwani.
‘’Mjisajili kwa Wakala wa Huduma za Misitu ili mpate fursa ya kuongeza kipato chenu, nyinyi ndio mnaostahili kwanza kwani misitu ipo kwenye maeneo yetu na ndio tunaitunza wenyewe hivyo nashangaa kuona wavunaji wengi wa mazao ya misitu wengi wanatoka nje ya Mkoa wetu wa Pwani’’amesema Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Eng. Evarist Ndikilo.
Mkoa wa Pwani unayo jumla ya misitu 34 ya hifadhi yenye jumla ya hekta 335,712 iliyohifadhiwa kisheria na hekta milioni 2.2 za misitu kwenye ardhi huria ambapo rasilimali hii ya misitu hutegemewa na kutumiwa na wakazi wa Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi ya nishati,mbao,magogo,samani na matumizi mengine.
By dkambanyuma
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa