Jumla ya vikundi thelathini na tano vyenye idadi ya wanachama 229 vimefanikiwa kupata mkopo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe
mkopo huo wenye thamani ya jumla ya kiasi cha shilingi milioni mia moja na elfu kumi na mbili na laki nane (112,800,000) unatoka kwenye mfuko wa maendeleo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambapo ni asilimia kumi ya mapato yanayokusanywa na Halmashauri kila mwaka.
Akikabidhi hundi za mikopo hiyo mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawla za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo, amesema Serikali imeamua kufanya kazi kwa vitendo zaidi ambapo kwa sasa Halmashauri zote Nchini zimetakiwa kutenga mapato asilimia kumi ya bajeti yake kila mwaka na kuwapa mikopo wanawake,vijana na watu wenye ulemavu bila riba.
‘’Mwaka huu wakati wa bajeti tulipeleka muswada wa sheria kuhusu mikopo inayotolewa na Halmashauri na bahati njema Bunge limepitisha muswada huo na kuwa sheria kwa hiyo kuanzia sasa mikopo inayotolewa na Halmashauri itatolewa kwa vikundi hivi pasipo kuwa na riba’’ amesema Mheshimiwa Jafo.
Katika awamu hii ya utoaji mikopo jumla vikundi vilivyokopeshwa ni thelathini na tano( 35) ambapo Wanawake ni vikundi 22 vyenye jumla ya wanachama 142 na kiasi walichokopeshwa ni shilingi Milioni hamsini na tatu na laki tano (53,000,000/=), vikundi vya vijana waliokopeshwa ni tisa vyenye wanachama `Hamsini na tisa ambapo wamekopeshwa jumla ya shilingi milioni arobaini na tisa na laki nane(49,800,000) na vikundi vya watu wenye ulemavu vilikuwa ni vinne vyenye jumla ya wanachama ishirini na nane na wamekopeshwa kiasi cha shilingi milioni tisa na laki tano(9,500,000)
Vikundi vilivyopata mikopo kwa awamu hii ya kwanza kwa mwaka huu vinajishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za viwanda vidogo vidogo kama vile utengenezaji wa masweta,batiki,vikoi,mafuta ya mgando,mikeka,usindikaji wa mvinyo na shughuli nyinginezo pia vikundi vingine vinajishughulisha na biashara ndogondogo kama vile magenge,migahawa, uendeshaji wa boda boda na kilimo.
Hafla ya makabidhiano ya mikopo imehudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa Pwani,mkuu wa wilaya ya kisarawe mheshimiwa Jokate Mwegelo,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Ndugu Mussa Gama, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kisarawe Ndugu Mtela Mwampamba,Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Hamisi Dikupatile, Kamati ya Fedha na Viongozi wengine wa Chama Cha Mapinduzi wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kisarawe ndugu Halfani Sika
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa