Shilingi Bilioni 10.9 Zasainiwa Kuleta Maji Kisarawe.
Jumla ya kiasi cha shilingi bilioni kumi na milioni mia tisa zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa ulazaji wa bomba la maji kutoka Kibamba kuelekea Kisarawe umbali wa takribani kilomita thelathini na tisa.
Katika hafla ya utiaji saini wa mradi huo mkubwa ulioshuhudiwa na mawaziri wawili wa serikali ambao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo (MB) na Waziri wa maji Mhe. Isack Kamwelwe,Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo,Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani Mhe Zainabu Vullu,Viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wa Kisarawe umeshudia mpango mahsusi wa kuleta maji kutoka bomba kuu la maji kutoka Ruvu linalopita pembezoni mwa barabara ya Morogoro kwenda kisarawe
Wakati wa Hafla hiyo iliyofanyika viwanja vya stendi ya Wilaya ya Kisarawe Waziri wa OR-TAMISEMI ambaye pia ni mbunge wa Kisarawe Mhe Selemani Jafo amesema ni furaha kubwa kuona kuwa hatimaye sasa Kisarawe inapata maji safi na salama ya kutosha kutoka Ruvu kwani itasaidia mji wa Kisarawe kubadilika na kuleta maendeleo.
‘’tuna furaha kubwa kwa ajili ya mradi huu kwani tuna eneo kubwa la viwanda ambalo limetengwa hivyo mradi huu ni fursa itakayowezesha eneo letu kubadilika kwani shida yetu kubwa ilikuwa ni maji’’ alisema Mhe. Selemani Jafo.
Vilevile Waziri wa maji Mhe kamwelwe amesema katika kutekeleza ilani ya chama tawala ni lazima watekeleze yale waliyoyaahidi kwa wananchi.Mradi huu wa ulazaji mabomba kutoka Kibamba kuja Kisarawe utawezesha kiasi cha maji lita takribani milioni nne kufika Kisarawe kwa siku na utachukua umbali wa kilomita 39 kulaza mabomba yenye ukubwa wa milimita 400 na mabomba yenye ukubwa wa milimita 80 hadi 200 kwa ajili ya usambazaji maji kwa wananchi na taasisi nyinginezo.
Tukio la utiaji saini lilifanywa baina ya Serikali kupitia kwa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Romanus Mwang’ingo na Mkandarasi aliyekabidhiwa ujenzi wa ulazaji mabomba ambaye ni kampuni kutoka nchini China inayojulikana kwa jina la China Henan International Cooperation GROUP ambapo kiongozi wake Ndugu Wang Xiaogang alihusika kwenye utiaji saini huo.
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa