Wananchi wa kijiji cha Yombo Lukinga kilichopo kata ya chole Tarafa ya chole Wilaya ya Kisarawe wametoa elimu ya kutosha kwa wataalam mbalimbali waliofika kijijini hapo kujifunza namna ya kuibua miradi na kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi.
Elimu hiyo imetolewa na Halmashauri ya kijiji ikiongozwa na Mwenyekiti wa kijiji pamoja na wataalamu waliopo kijijini hapo kwa wataalam kutoka Ofisi ya Rais Tawala Za Mikoa na Serikali Za Mitaa (TAMISEMI) Walioambatana na ujumbe kutoka shirika la Misaada kutoka Japan (JICA) ambapo wamejifunza namna ya ushirikishaji wananchi kwenye kuchangia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayowahusu wananchi wenyewe.
Katika mafunzo hayo wajumbe wa Halmashauri ya kijiji cha yombo Lukinga wamebainisha kuwa uongozi bora unaowashirikisha wananchi ndio chachu ya mafanikio waliyo nayo ambapo wananchi wanajenga Imani na matumaini kwa viongozi wao kiasi cha kuwawezesha wao kuchangia kwa hali na mali miradi inayopendekezwa kutekelezwa kwenye kijiji chao.
Kijiji cha Yombo Lukinga kimefanikiwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo hapo awali kwao ilikuwa ni changamoto kubwa kwa ustawi wa jamii yao. Wananchi wameweza kuibua na kutekeleza ujenzi wa shule ya msingi ili watoto wao waweze kujifunza .
Pia wameibua na kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa Zahanati ya kijiji na mpaka sasa ujenzi huo bado unaendelea kwa wananchi kujitolea na serikali imeendelea kuwaunga mkono katika kutekeleza sera ya mkono kwa mkono.
Aidha wajumbe wa Halmashauri ya kijiji cha Yombo Lukinga wamepongeza na kushukuru uungwaji mkono wa kiwango cha juu unaofanywa na Halmashauri ya wilaya katika kufanikisha kutekeleza miradi inayoibuliwa na wananchi ambapo katika mradi wa ujenzi wa madarasa Halmashauri ya Wilaya imechangia kwa kiasi kubwa pia wanaendelea kuchangia ujenzi wa zahanati unaoendelea.
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa