MILIONI 102,204,000/= ZATOLEWA KWA VIKUNDI VYA VIJANA,WANAWAKE NA WATU WENYE ULEMAVU.
Halmashauri ya Wilaya ya kisarawe imefanikiwa kutoa kiasi cha shilingi milioni mia moja na mbili lakimbili na elfu nne ikiwa ni 10% toka mapato yake ya ndani kwa vikundi vya wajasiriamali vya Wanawake,Vijana na Walemavu ili kuweza kuwasaidia kuondokana na umasikini kwa kuwaingizia kipato.
Zoezi la utoaji fedha hizo limefanyika siku ya Jumanne tarehe 21/11/2017 kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mheshimiwa Happiness Seneda na kuhudhuriwa na wanavikundi zaidi ya 411 pamoja na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali.
Akiongea katika zoezi hilo Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Happiness Seneda amewapongeza wanavikundi na kuwaasa kutumia fedha walizokopeshwa kwenye malengo yaliyokusudiwa na kuwahamasisha waongeze juhudi ili waweze kusonga mbele na hatimaye waweze kukua na kuweza kupata mikopo mikubwa kutoka katika Taasisi za fedha kama vile benki.
Vilevile Mkuu wa Wilaya amewaasa wanavikundi kurejesha fedha walizokopa ili iweze kuwezesha mfuko uwe na fedha nyingi zinazozunguka ikiwezekana ifike hadi shilingi milioni mia tano.’’Hii ni fedha ya kukopa na sio msaada,hii ni fedha iliyotolewa kwa ajili ya miradi iliyokusudiwa na siyo ya kununulia madela,sare au kucheza ngoma” amesema Mheshimiwa Hapiness Seneda.
Jumla ya vikundi 49 vyenye wanachama 411 vimepitishwa na kupewa mikopo ya jumla ya shilingi 102,204,000/= ambapo vikundi 41 vya wanawake vimepewa kiasi cha shilingi 73,500,000/= ,vikundi vya vijana 7 ambavyo vimepewa shilingi 26,704,000/= na kikundi kimoja cha Walemavu kimepata mkopo wa shilingi 2,000,000/=.
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa