Mazingira ni jumla ya mambo na vitu vyote vinavyomzunguka kiumbe hai.Hii inamaanisha kuwa kila kitu kinachomzunguka kiumbe hai na kinachosababisha uwepo na uendelezaji wa uhai ni mazingira.
Viumbe hai vinategemea mazingira,hata viumbe visivyo hai pia hutegemea mazingira yaani inajumuisha ardhi ,maji,hewa uoto, na vinginevyo ambapo kwa umoja wake unasababisha uhai uwepo na uendelee.Kwa misingi hii ni wajibu wetu kupambana kuhifadhi na kulinda mazingira endapo tunahitaji kuishi na kuendeleza uhai kwa vizazi vijavyo.
Juhudi tunazoziimarisha na kuamsha ari kubwa miongoni mwetu kwa wanajamii katika kulinda mazingira kunaakisi umuhimu na tija katika maendeleo ya viwanda.
Madhara makubwa ya kuendelea kuharibu mazingira yetu na athari zitokananzo na uharibifu huu zinafanya jamii zetu zipate maumivu ambayo yanasababishwa na sisi wenyewe kutokana na ukosefu wa maarifa, ujinga na kutojali ingawa athari zake hazihitaji kutumia darubini kutambua kuwa tumetafuta majanga haya wenyewe.
Tujiulize kwa nini watu wanaharibu mazingira? Kitu gani kinasababisha tuharibu mazingira yetu? Je ni jinai kuharibu mazingira yetu ? Ukweli usiojificha ni kuwa ukataji wa miti usiozingatia sheria ni mwiba mchungu kwa maendeleo ya taifa hili.
Takwimu zinaonyesha kuwa kwa siku moja zaidi ya ekari elfu kumi (10,000) zinaharibiwa kwa ajili ya matumizi ya mkaa na matumizi mengine hapa nchini. Asilimia tisini (90%) ya watanzania wanatumia mkaa ambapo asilimia themanini na tano (85%) ya matumizi ya mkaa huo hutumiwa na wakazi wanaoishi jijini Dar es Salaam.
Zipo sababu zinazofanya watanzania wengi watumie nishati ya mkaa na baadhi yake ni utamaduni na mazoea . Mazoea katika kutumia nishati ya mkaa huamini kuwa mkaa huivisha chakula vizuri kama maharage,wali nk.kulinganisha na nishati ya gesi au umeme.mazoea/utamaduni haya hupelekea hata watu wenye kipato cha kati kupendelea kutumia nishati hii japo inaharibu mazingira.
Sababu nyingine inayochangia watu waendelee kutumia nishati ya mkaa ni nguvu ya soko (biashara) ambapo soko la mkaa ni jepesi na ni rahisi kuiendesha kulingana na mazingira yetu na pia ni rahisi kwa gharama kulinganisha na nishati nyinginezo jambo ambalo si la kweli kiuhalisia
Kipato duni ni sababu nyingine kwani nishati mbadala imeonekana ni ghali sana hali hii hupelekea watu wengi kutumia mkaa na ukweli ni kwamba kipato cha watanzania wengi hasa wale wa maeneo ya ya vijijini ambao ndio watumiaji wakubwa wakubwa wa nishatiya kuni na mkaa.
Pamoja na sababu zote zilizoorodheshwa zinazosababisha ukataji wa mkaa bado sisi kama wana mazingira hatuziafiki na hatukubaliani nazo, kwani zipo njia nyingi na rahisi ambazo tukitumia tunaweza kutimiza mahitaji yetu na pia kulinda mazingira.
Njia rahisi ni kutumia nishati mbadala.Nishati ambazo haziwezi kuharibu mazingira na zimependekezwa na wanamazingira na wataalamu kuwa zinafaa.Nishati hizo zaweza kuwa Nishati ya gesi, Nishati ya jua (Solar power), Umeme, Bayogesi (nishati inayotokana na uozo wa masalia mbalimbali ya vyakula na hata vinyesi vya wanyama) na nishati ya mkaa unaotokana na masalia ya uchafu/takataka za nyumbani mfano vifuu vya nazi,pumba za mbao,maganda ya korosho na mabunzi ya mahindi.
Napenda kunukuu kauli ya mwalimu ambaye pia alikuwa ni Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Julius Nyerere kuwa ‘’Elewa kuna kitu kinaitwa wizi,wizi wote ni mbaya,lakini wizi mbaya kupita wote ni kumuibia mtoto wako ambaye hajazaliwa,ni kumuibia mjukuu,unaiba mali yake.Na kuharibu mazingira ni kuiba mali ya vizazi ambavyo havijazaliwa.Wewe umekuta mlima ule una miti mizuri,umerithishwa wewe na wale waliokutangulia,wamekupa mazingira mazuri ya miti yana miti mizuri,inaleta hewa nzuri na inasaidia kuleta mvua.Wewe kwa ujinga wako unaharibu miti ile,watoto wako na wajukuu wako wanaokuja baadae wanakuta hali si nzuri kama uliyokuwa nayo,Umewaibia!Mwizi weye!Mwizi! Tupande miti!!’’
Mikakati yetu wanamazingira,hasa tunaotoka maenea ambayo yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira hasa unaotokana na mkaa .Sisi wana wa Kisarawe Mkoa wa Pwani tumeazimia kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za matumizi ya mkaa,uundaji wa vikundi vidogo vidogo vya mazingira katika vitongoji na mashuleni na kamati ndogo za moto za vijiji.
Pia kuweka mikakati ya pamoja kwa kushirikiana na taasisi nyinginezo mfano TFS,WWF,Wizara ya Nishati na Madini NG’Os na CBO’s na kufanya makongamano mbalimbali katika kuhamasisha jamii juu ya matumizi bora ya nishati mbadala.
Kuwatambua wadau wanaotoa mchango wa kutunza na kuhifadhi mazingira kiwilaya ili kuweza kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za simamizi na uhifadhi wa mazingira ikiwezekana kuwapa motisha.
Halmashauri kushirikiana na wizara yenye dhamana ya mazingira na maliasili kuyatambua na kutenga maeneo ya hifadhi ili kunusuru uoto na ikolojia yake isiendelee kuharibiwa.
By dkambanyuma
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa