Sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 ilipitishwa na bunge la Jamhuri ya Muugano wa Tanzania mwezi april 2010 na kusainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 mei 2010.
Tujiulize? Hata kwa sauti tuwaze! Ni nani haswa anayepaswa kusimamia sheria hii? Je ni bunge ambalo ndio waliotunga sheria hii? Je ni serikali au Mahakama ambayo kisheria na kimamlaka ndio wasimamizi wakubwa wa sheria zetu tunazozitunga? au ni jamii ambayo tunaguswa na changamoto hizi au ni walemavu? NINI TUFANYE?
Kwanza sisi tukiwa jamii inatupasa tutambue tangu awali viashiria vya utambuzi wa watoto wenye ulemavu,Hii itasaidia kuweza kujua mapema athari zilizopo na pengine kuweza kuepuka au kupunguza athari kwani baadhi ya matatizo ya ulemavu yanaweza kutibika na kuepukika iwapo utambuzi utafanyika mapema kwa watoto.
Ulemavu ni hali inayotokana na upungufu katika viungo vya mwili,vya akili na milango ya fahamu ambayo inampunguzia mtu uwezo na fursa hasa hali hiyo inapokutana na vikwazo katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika jamii.
Katika hali ya kuthaminiana,kujali utu na heshima ya mwanadamu ambapo watanzania ndiyo jadi yetu, suala linalotugusa jamii bila kujali itikadi,rangi kabila wala imani tunapaswa kuwajibika kwa pamoja na sio suala la kuwaachia taasisi,asasi, kikundi au serikali kuwajibika katika kulinda na kutetea maslahi ya kundi Fulani lenye mahitaji bali ni sote kwa pamoja.
Sheria ya watu wenye ulemavu imewekwa ikiwa na lengo la kuweka mwongozo wa kisheria wa namna ya utekelezaji utoaji huduma kwa watu wenye ulemavu,kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa wanajamii juu ya haki za watu wenye ulemavu na kuchangamana na kushirikiana katika mazingira mbalimbali ya kazi ,kijamii na fursa za kiuchumi,
Pia kukuza uelewa miongoni mwa jamii juu ya wajibu na majukumu ya kila mwananchi na mamlaka mbalimbali za kijamii kuhakikisha haki na fursa za watu wenye ulemavu zinaimarishwa ili kujenga jamii jumuishi inayowakubali watu wa aina zote.
Mara nyingi kunapotokea tukio la kuwakutanisha pamoja watu wenye ulemavu na wale wasio walemavu ni dhahiri jamii ya wasio na ulemavu tumeshuhudia wakisononeshwa na kuhuzunishwa na hali waliyo nayo walemavu.Basi kama ndivyo, huzuni hii isiwe inaishia kwa kuwaonea huruma tu bali pia itukumbushe wajibu wetu wana jamii jukumu la kuhakikisha tunawahudumia , kushirikiana na kuchangamana nao si kwa sababu sheria imetaka iwe hivyo bali ni hiari ya lazima ya kutimiza wajibu wetu kutoka ndani ya mioyo yetu .(nafsi zetu)
Nafsi zetu zitukumbushe kuwa tuna wajibu wa kukomesha ubaguzi na kuleta usawa,wajibu wa kutoa msaada wa kijamii kwa watu wenye ulemavu,wajibu wa kuwalinda na wajibu wa kutoa ajira na kuendeleza ajira kwa watu wenye ulemavu.
Katika kutekeleza wajibu na matakwa ya sheria hii inatupasa sote kwa pamoja tuwajibike huku tukiwa na furaha mioyoni mwetu kwa tendo la kishujaa tunalofanya kama ilivyo kwa baadhi ya taasisi.asasi na serikali inavyawajibika katika hili.
Mfano Hai,Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe iliyopo Mkoa Pwani imedhamiria na kuanza kutekeleza wajibu wake kwa kuwapatia watu wote wenye ulemavu Wilaya ya Kisarawe bima ya afya ambayo itawawezesha walemavu kupata matibabu bure kwenye Zahanati,Vituo vya afya na Hospitali zilizopo Wilaya ya Kisarawe.
Kitendo hiki kitapunguza mzigo mzito waliokuwa nao walemavu katika kugharamia huduma ya matibabu kwani kama tunavyojua gharama za matibabu ni ghali sana si kwa walemavu pekee bali hata kwa watu walio na utimamu wa viungo na akili.
Kwa kuhitimisha napenda kunukuu kauli ya mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya walemavu Tanzania SHIVYAWATA bi Ummy Nderiananga kama ifuatavyo’’Niwageukie wenzangu wenye ulemavu,kwa vipawa tulivyojaaliwa na mwenyezi mungu naomba tujitaidi kuzichangamkia fursa zilizopo katika maeneo yetu.Nawatia moyo nikiwaambia kuwa tunaweza, sisi viongozi wenu tupo pamoja nanyi’’
SISI tunawapenda,tunawajali na kuwalinda .Ndugu zangu, walemavu wasioona,viziwi,walemavu wa ngozi,walemavu wa akili,viungo, wagonjwa wa akili,walioumia uti wa mgongo na walemavu wa Mbalanga mbalanga Chepechepe tunawapenda, tuchangamkie fursa zilizopo mbele yetu kwani nguvu zenu kwa umoja wenu ni chachu kwetu jamii nzima ya Watanzania .
By dkambanyuma
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa