Wanafunzi 2848 Wafanya Mtihani Wa Utamilifu’Mock’ Wilaya Ya Kisarawe.
Wanafunzi wa darasa la saba wanaosoma katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe wanafanya mitihani ya Utamilifu ngazi ya Wilaya ulioanza kufanyika leo siku ya alhamisi tarehe 17.05.2018
Jumla ya wanafunzi 2848 wameshiriki kufanya mtihani huo ambapo wanafunzi wasichana ni 1469 na wavulana 1379 na jumla ya shule za msingi zinazohusika kwenye mtihani huo ni themanini na saba ambapo shule za serikali ni themanini na tatu na shule binafsi ni nne.
Wakati wa mtihani huo wanafunzi wa shule ya msingi Mlegele wamesema wamejiandaa vyema na walimu wamejitahidi kuwatayarisha vyema hivyo wanatarajia kupata alama nzuri
‘’ Mtihani ni wa kawaida ,kutokana na walimu walivyotuandaa vizuri na juhudi tunazofanya wenyewe nina uhakika tutapata alama nzuri sana ‘’ alisema Salehe Ally ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba anayefanya mtihani huo.
Afisa elimu wa Wilaya ya Kisarawe ndugu Shomari Bane amesema mitihani hii inawaandaaa vijana kuhimili vishindo vya mtihani wa mwisho wa Taifa ambapo kwa mwaka huu tumejipanga kufanya mitihani miwili ambao wa kwanza ndio tunafanya sasa na mwingine tunatarajia kufanya mwezi wa saba.
Aidha Afisa Elimu amesema pia kutakuwa na mtihani wa utamilifu ngazi ya Mkoa utakaofanyika muhula wa pili mwaka huu kabla ya mtihani wa mwisho wa kumaliza elimu ya msingi unaotarajiwa kufanyika mwezi wa tisa.
Mtihani wa utamilifu ngazi ya wilaya ya kisarawe umeanza kufanyika leo siku ya Alhamis tarehe 17.05.2018 na utamalizika siku ya Ijumaa tarehe 18.05.2018 ukiwa na lengo la kuwaandaa wanafunzi wa darasa la saba kukabiliana ipasavyo na mtihani wakumaliza elimu ya msingi mwezi wa tisa mwaka huu.
By dkambanyuma
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa