Na.kambanyuma David
Zaidi ya wagonjwa laki tatu wanaopata huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe wanatarajia kunufaika na huduma bora za afya zilizoboreshwa baada ya Hospitali hiyo kupatiwa vifaa tiba Zaidi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa.
Akikabidhi vifaa tiba hivyo kwa hospitali ya Wilaya ya Kisarawe Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Mb) Mheshimiwa Selemani Jaffo amesema serikali inajitaidi kwa kila hali kuboresha miundombinu na vifaa tiba kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akisoma taarifa fupi kuhusu utoaji wa huduma katika Hospitali ya Wilaya Mganga Mkuu wa Wilaya Ya Kisarawe Dokta Jonathani Budenu amesema hospitali ya Wilaya inapokea wagonjwa kutoka katika vituo vya afya na zahanati baada ya kushindikana matibabu ngazi ya zahanati na vituo vya afya.Kwa sasa inahudumia Zaidi ya wagonjwa laki tatu kwa mwaka.
Aidha Mganga Mkuu amesema katika kutatua changamoto na kuimarisha utoaji wa huduma ,timu ya usimamizi wa huduma za afya ya Wilaya pamoja na timu ya usimamizi ya Hospitali wametumia vyanzo mbalimbali vya fedha ili kutatua changamotohizo kwa kununua vifaa mbalimbali vilivyogharimu kiasi cha shilingi milioni mia moja na kumi na tisa (119,500,000/=).
Vifaa vya uchunguzi vilivyonunuliwa kwa ajili ya utoaji huduma za afya ni pamoja na mashine ya ultra sound iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni arobaini na sita( 46,000,000/=),mashine ya kutoa dawa ya usingizi shilingi milioni thelathini na moja (31,000,000/=),Haematology analyser shilingi milioni ishirini na mbila na laki tano(22,500,000/=) Water bath,Chemistry analyser,Baby warmer na Incubator ya maabara ambapo upatikanaji wa vifaa hivi umetumia fedha za RBF, Cost Sharing na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Pia Hospitali ipo katika mipango ya kuimarisha usimamizi na utoaji wa huduma za afya kwa kupanua wodi ya wazazi,upasuaji, kuanzisha kitengo cha Dharura,kujenga jengo la wagonjwa wa nje ‘OPD’,kuanzisha Infusion Unit na kutumia mfumo wa ukusanyaji wa mapato wa kielektroniki kupitia benki ya CRDB.
Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe inapokea wagonjwa kutoka katika vituo vya afya vya Maneromango,Chole,Mzenga,Masaki na wagonjwa wanaotoka nje ya Wilaya ya kisarawe kutoka wilaya ya Ilala iliyopo Mkoa wa Dar es salaam.
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa