Kamati Ya Fedha Kisarawe Yatembelea Miradi
Kamati ya fedha Halmashauri ya Wilaya ya kisarawe ikiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mheshimiwa Hamisi Dikupatile imetembelea miradi mbalimbali inayoendelea na ujenzi katika Wilaya ya Kisarawe.
Katika ziara hiyo imejumuisha wajumbe wa kamati hiyo ambao ni baadhi ya waheshimiwa madiwani, katibu wa kamati ambaye ni kaimu mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Ndugu Patric Allute pamoja na Wataalamu wametembelea miradi ya ujenzi wa Zahanati kijiji cha Kibwemwenda kata ya Vihingo,Kituo cha Afya Mzenga na ujenzi wa madarasa shule ya Sekondari ya Gwata.
Awali wakikagua ujenzi wa Zahanati ya kibwemwenda kamati ya fedha ilishuhudia maendeleo ya ujenzi huo ambao mpaka sasa wameshakamilisha kazi ya kupaua na wanatarajia kumaliza kazi iliyobaki hivi karibuni.
Aidha mwenyekiti wa Halmashauri amewapongeza kwa juhudi wanazoendelea nazo na kuwaambia hivi punde pesa ya umaliziaji wa ujenzi itatolewa na anatarajia ujenzi utakamilika mapema ili zahanati iweze kutoa huduma kwa wananchi.
Katika kituo cha Afya cha Mzenga kamati ya fedha ilikutana na kamati ya ujenzi ya zahanati hiyo na ilishuhudia maendeleo ya ujenzi huo ambao upo katika hatua za mwisho za umaliziaji ili uweze kutumika na kamati imejiridhisha kwa hatua iliyofikiwa mpaka sasa.
Pia kamati ya fedha imetembelea shule ya sekondari ya Gwata kukagua mradi wa ujenzi wa madarasa pamoja na shughuli nyinginezo zinazofanyika shuleni hapo pamoja na kukutana na uongozi wa shule na kutoa ushauri namna ya kubboresha miundombinu wezeshi ya kujifunza na kujifunzia.
Vilevile kamati ilitembelea machimbo ya kokoto yaliyopo kijiji cha kibwemwenda kata ya Vihingo ambapo kokoto hizo zinatumika katika ujenzi wa mradi wa reli ya Treni ya KIsasa (SGR) na kuona namna ya shughuli za uchimbaji mawe unavyoendelea.
Kamati ya Fedha inaundwa na wajumbe ambao ni waheshimiwa madiwani kutoka kata za Maneromango,Msimbu,Msanga,Marui,Mzenga na Kiluvya ambaoni Mheshimiwa Hamisi Abdallah,Mhe.Amina Lilomo,Mhe. Juma Kizwezwe,Mhe.Salehe Mfaume,Mhe.Mohamed Lubondo na Mhe. Aidan Kitare pamoja na Diwani wa viti maalum Mhe, Tatu Kano na Mbunge wa jimbo la Kisarawe Mheshimiwa Selemani Jafo.
Aidha wataalam wa Halmashauri walioongozana na kamati ya Fedha ni Mkuu wa idara ya ujenzi Mhandisi Mahungo,Afisa elimu Sekondari Ndugu Generosa Nyoni,Kaimu Afisa elimu Msingi Ndugu Madina Mussa, Kaimu Afisa Mipango,Takwimu na Ufuatiliaji Ndugu Deus Mbalamwezi,Kaimu Mkaguzi wa Ndani Ndugu Sadikiel Mnzava, Afisa Habari Ndugu David Kambanyuma na Mwandishi wa vikao Ndugu Emmanuel Mgonja.
Hakimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. Haki zote zimehifadhiwa